Monday, July 9, 2012

ASHA ROSE MIGIRO ATOA WARAKA MZITO

ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk Asha-Rose Migiro ambaye anarejea nchini leo ametoa waraka maalumu akisema mwisho wa utumishi wake katika umoja huo ni mwanzo utekelezaji wa majukumu mengine hapa nchini.
Kauli ya Dk Migiro imekuja kipindi ambacho jina lake limekuwa likitajwa katika nafasi ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete atakapomaliza muda wake wa kuongoza taifa mwaka 2015. Kabla ya kwenda UN, Dk Migiro alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Dk Migiro ambaye aliteuliwa na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-Moon kushika mwaka 2007 wadhifa huo, alisema anafurahi kumaliza miaka mitano kwa mafanikio.
Katika waraka huo ambao gazeti hili limeuona jana, Dk Migiro alisema: “Hakika, kila chenye mwanzo hakikosi mwisho na kila mwisho wa jambo moja huwa mwanzo wa jingine.”
Alisema ingawa ni mapema kwake kutoa tathmini halisi ya utendaji wake kazi, wadhifa huo katika Umoja wa Mataifa umempatia uzoefu mkubwa.
“Kukitumikia chombo hiki cha kimataifa kwa muda wa miaka mitano na nusu mfululizo ni heshima ya pekee ambayo daima nitaienzi  kama kilele kimojawapo  cha mafanikio katika maisha yangu ya utumishi  wa umma. Kila siku niliyoitumia katika Umoja huo ilikuwa ni darasa la kusukuma mbele mipaka ya ujuzi na elimu,” alisema Dk Migiro.
Alisema amefahamu mambo mengi kuhusu umoja huo, dunia na watu wake ikiwamo ukomo  wa umoja huo katika kushughulikia matatizo mbalimbali yanayoikabili dunia.
“Daima nitaendelea kushukuru na kuthamini kwa dhati jinsi Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Serikali na Watanzania wenzangu walivyonitia moyo na kunienzi katika kipindi chote nilichokuwa Umoja wa Mataifa,” alisema.
Dk Migiro alisema utumishi wake katika umoja huo ulikuwa fursa adhimu iliyompa uzoefu wa kipekee hasa ikizingatiwa kwamba aliingia wakati ukikabiliwa na changamoto kubwa zikiwamo za maradhi, umaskini wa kupindukia na vitendo vya kikatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto.
Alisema matatizo hayo na mengine yalimpa fursa ya kuchangia kikamilifu jinsi ya kukabiliana nayo wakati akitekeleza majukumu yake.
Dk Migiro alisema umoja huo umemwezesha kufahamiana na viongozi wengi wa kimataifa na watu mbalimbali wenye mafanikio duniani.... “Nimeweza kufahamu kwa undani thamani ya michango yao katika kujenga amani na ustawi wa dunia."
Alisema ingawa muda wake wa utumishi umekwisha kwenye umoja huo, ataendelea kuunga mkono jitihada za UN za kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia.
Sitasahau
Akizungumzia mambo aliyowahi kukutana nao katika utumishi wake, Dk Migiro alisema hatasahau hisia alizozipata kila alipokutana na watu wanyonge waliokuwa wanahitaji msaada wa Umoja wa Mataifa.
“Nitakumbuka daima tabasamu la mwanamke mmoja niliyekutana naye katika moja ya ziara zangu barani Afrika nilipotembelea zahanati mojawapo kati ya kadhaa zinazofadhiliwa na Umoja wa Mataifa,” alisema na kuongeza:
“Mama huyo mwenye watoto sita, alikuwa amekikumbatia kitoto chake kimoja kilichokuwa na afya dhaifu kwa kuumwa lakini alikuwa na tabasamu iliyojaa faraja na matumaini kwa kuwa alikuwa amefanikiwa kupata bure dawa za kunusuru maisha ya mwanawe.”
Alisema mama huyo pamoja na matatizo aliyonayo ya kuuguliwa na mwanaye, alipata faraja baada ya kuwa na uhakika wa kupata matibabu kwenye zahanati hiyo ya UN.
Dk Migiro alisema katika utekelezaji wa majukumu mengine, nguvu nyingi zilielekezwa katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) na mengine yaliyokubaliwa kimataifa.
“Nilihamasika sana na dhamira waliyoionyesha wadau na washirika wetu wa maendeleo, zikiwemo Serikali, mashirika ya kiraia na mashirika ya biashara katika kufikia malengo ya milenia,” alisema.
Alisema anamaliza kipindi chake kukiwa na maendeleo mazuri yanayotokana na jitihada za kimataifa za kupambana na umaskini akisema mikakati ya UN ya kutaka kupunguza idadi ya watu maskini duniani kufikia angalau nusu ya viwango vya sasa, zimeanza kuzaa matunda.
“Taarifa hii ni ya kutia moyo licha ya ukweli kwamba dunia inapitia matatizo makubwa ya kiuchumi kuliko wakati mwingine wowote uliowahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni,” alisema Dk Migiro katika waraka wake.
Dk Migiro alisema wakati wa utumishi wake katika umoja huo, ametumia nguvu kubwa na hadhi ya ofisi yake katika kupaza sauti za wanawake na wasichana ili kuleta usawa wa kijinsia.
“Tumeendesha kampeni za kupiga vita ukatili kwa wanawake na wasichana. Tumezihimiza mamlaka katika ngazi za kitaifa na kimataifa kutunga sera na sheria zinazozingatia haki za wanawake na usawa wa kijinsia na tumetaka wapewe fursa kushika nafasi za uongozi katika jamii,” alisema.
Alisema ili kufanikisha hilo, umoja huo ulifikia uamuzi wa kuanzisha idara ya umoja wa mataifa kwa madhumuni ya kuongoza masuala ya wanawake na masuala ya kijinsia.
“Tumefanya jitihada hizi kwa kuamini kuwa hakuna uamuzi wowote ule, uwe mdogo au mkubwa, unaofanywa na Umoja wa Mataifa bila ya kuzingatia maendeleo na ustawi wa wanawake na wasichana,” alisema.
Alisema katika eneo la afya ambako wanawake na watoto ndiyo wanaathirika wakubwa, juhudi zinafanywa kupunguza vifo na kuhakikisha kwamba kila mwanamke na mtoto anakingwa na maradhi ikiwamo kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Alisema mwaka 2011, akiwa katika ziara jijini Nairobi, Kenya na Katibu Mkuu, Ban Ki-Moon  walipata fursa ya kukutana na mwanamke aliyeathirika na Virusi vya Ukimwi ambaye alijifungua watoto pacha watatu waliozaliwa bila ya kuambukizwa.
Tulifurahishwa na mpango wa kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa,” alisema Dk Migiro.
Alisema umoja huo umekuwa ni mtetezi wa wanyonge na wenye kutaabika sehemu zote duniani na kwamba watumishi wake wanafanya kazi katika mazingira hatarishi kwa sababu hivi sasa bendera ya bluu si kinga tena akisema baadhi yao  wamekuwa wakiuawa katika matukio mbalimbali.
“Bendera ya buu haituhakikishii usalama kwani wengi wa watumishi wetu mahiri wamekuwa waathirika wa matukio ya kikatili ya ugaidi. Nilishuhudia tukio la aina hii huko Abuja, Nigeria ambako watumishi wenzetu walipoteza maisha kutokana na shambulio la kigaidi la Agosti 26, 2011,” alisema.
Alisema mara nyingi watumishi wa umoja huo wanapopoteza maisha, familia zao zinaachwa katika hali ngumu na kwamba kabla hajamaliza muda wake alianzisha mchakato wa kubaini namna bora ya kuwasaidia waathirika wa majanga hayo pamoja na familia zao

No comments:

Post a Comment