Ndugu Wananchi;
Tarehe
27 Juni, 2012 nilikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama
nchini kuzungumzia tukio la Chitego na suala zima la biashara hii haramu
na hasa mbinu mpya inayotumiwa na wasafarishaji. Nilitoa pongezi kwa
vyombo vya dola kwa kazi nzuri waifanyayo kudhibiti shughuli za biashara
hii haramu hapa nchini. Tulielewana kuwa waendelee kuimarisha udhibiti huo kwa lengo la kukomesha kabisa biashara hii.
Niliagiza pia kwamba kikundi kazi nilichokiunda mwaka 2006
kushughulikia ujambazi sasa kielekeze sehemu ya nguvu zake kukabili
tatizo hili. Aidha, kwa pamoja tulikubaliana kuwa nchi yetu ishirikiane
na wenzetu wa Ethiopia, Kenya, Malawi, Msumbiji na Afrika ya Kusini
kutambua mawakala na kuwabana kwa mujibu wa sheria. Tayari nimeshaanza
kufanya mawasiliano na baadhi ya Wakuu wa Nchi hizo kuhusu ushirikiano
huo. Nashukuru wote wameafiki nchi zetu zishirikiane kwa pamoja kuvunja
mtandao huu mchafu na kutokomeza biashara hii haramu na inayodhalilisha
utu wa mwanadamu.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuchukua nafasi hii kuwashukuru wenzetu, wakazi wa vijiji vya Chitego
na Mkoka kwa kazi nzuri walioifanya. Kwa kweli, wenzetu wameonesha
uzalendo wa hali ya juu kwa kutoa taarifa mapema juu ya jambo lenyewe,
lakini pia wameonesha utu kwa kuwajali wageni waliokumbwa na janga hili.
Naushukuru pia uongozi wa Mkoa wa Dodoma na Morogoro ikiwa ni pamoja na
vyombo vya ulinzi na usalama kwa kulishughulikia tatizo hilo kwa
umakini mkubwa. Nimefurahishwa sana na ushirikiano ulioonyeshwa na
vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali katika kushughulikia suala
hili.
Mgomo wa Madaktari
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ni kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini hivi
sasa. Nilipozungumza na Wazee wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond
Jubilee tarehe 12 Machi, 2012, kuhusu mgomo wa Madaktari uliokuwa
unaendelea wakati ule pamoja na kuelezea chimbuko la mgomo na hatua
iliyokuwa imefikiwa, nilielezea mazungumzo yangu na viongozi wa Chama
cha Madakari wakiwemo pia viongozi wa Jumuiya ya Madaktari. Nilitoa
taarifa kuwa tumeelewana kuwa
watasitisha mgomo na watarudi kwenye meza ya majadiliano na Serikali.
Siku ile pia nilielezea matumaini yangu kuwa mgomo ule utakuwa wa mwisho
katika nchi
yetu. Bahati mbaya matumaini yangu hayo hayakuwa na hivi sasa
tunashuhudia tena wagonjwa wakiteseka, kuhangaika na wengine kufa kwa
sababu ya kukosa huduma wanazostahili kwa vile madaktari wao wamegoma
tena.
Ndugu Wananchi;
Kama
walivyoniahidi, madaktari waliacha kugoma na viongozi wao walirudi
kwenye mazungumzo na Serikali. Kama ilivyoagizwa na Mahakama Kuu,
Kitengo cha Kazi tarehe 8 Machi, 2012, kwa mujibu wa Sheria ya Mahusiano
Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004. Chama cha Madaktari na Serikali
walifika katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (Commission for Mediation
and Arbitration) kwa ajili ya majadiliano. Kwa pamoja na kwa ridhaa yao
wote, pande hizo mbili ziliiomba Tume hiyo iwape fursa ya kuzungumza
wao wenyewe na wakimaliza mazungumzo wataenda kusajili makubaliano yao.
Tume ikawakubalia. Ni vizuri ikakumbukwa kuwa siku ile ya tarehe 8
Machi, 2012 Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ilitoa zuio la mgomo pamoja
na kuagiza kuwepo mazungumzo baina ya pande mbili.
Ndugu Wananchi;
Kati
ya tarehe 10 Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika vikao
sita vya majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari. Katika
mazungumzo hayo hoja au madai 12 ya madaktari yalizungumzwa. Mambo hayo
ni haya yafuatayo:
1. Posho ya kuitwa kazini (on call allowance) iwe asilimia 10 ya mshahara.
2. Posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (Risk allowance) iwe asilimia 30 ya mshahara.
3. Madaktari wapatiwe nyumba grade A au posho ya makazi ambayo iwe asilimia 30 ya mshahara.
4. Posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu iwe asilimia 40 ya mshahara.
5. Madaktari walipwe posho ya usafiri ya asilimia 10 ya mshahara au wakopeshwe magari.
6. Madaktari wanaoanza kazi walipwe mshahara wa shilingi 3,500,00/= kwa mwezi.
7. Madaktari wapatiwe Green Card za Bima ya afya.
8. Hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
9. Viongozi wa Kisiasa kulazimisha kupewa rufaa nje.
10. Madaktari waliofukuzwa warudishwe kazini.
11. Huduma za afya ziboreshwe nchini.
12. Posho ya uchunguzi wa maiti iongezwe.
Ndugu Wananchi;
Katika mambo hayo 12 pande zote mbili zilifikia muafaka na kukubaliana wa pamoja kwa mambo saba. La kwanza, ni kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi kazini. Serikali ilieleza
kuwa upo utaratibu kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3
wa mwaka 2011 wa kuwakopesha wafanyakazi wa Serikali fedha za kununulia
magari au pikipiki, samani na matengenezo ya magari. Ilikubaliwa kuwa
madaktari waitumie fursa hiyo.
Jambo la pili,
ni kuhusu madaktari kupatiwa Green Card za Bima ya Afya. Jambo hili
lilikubaliwa na Serikali na Wizara ya Afya imekwishachukua hatua za
utekelezaji wake.
Jambo la tatu, ni kuhusu hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya. Kwa pamoja walikubaliana kuwa suala
hilo liko nje ya mamlaka ya Kamati yao ya pamoja, waziachie mamlaka
husika za uteuzi. Uongozi wa juu wa Wizara umebadilishwa na sasa kuna
uongozi mpya.
Lakini, jambo la kustaajanisha hata Waziri mpya wa Afya alipowataka
waonane kuzungumzia hoja walikataa kumuona. Kwanza walisema hawaoni
sababu kwa vile wameyazungumza na Kamati yake kwa miezi mitatu bila ya
mafanikio
Jambo la nne walilokubaliana ni kuhusu viongozi kulazimisha kupewa rufaa ya kutibiwa nje. Walikubaliana mambo mawili. Kwanza,
kwamba maelekezo ya Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda kuwa madaktari
wazingatie maadili ya kazi zao na kukataa kutoa rufaa kwa mtu
asiyestahili awe kiongozi au asiwe kiongozi. Pili, walikubaliana kuwa hospitali zilizopo ziboreshwe ili viongozi watibiwe hapa nchini. Ukweli ni kwamba
kufanya hivyo ndiyo sera ya Serikali. Nililieleza hili mwezi Desemba
30, 2005 katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza nchi yetu.
Tumeiongeza sana bajeti ya sekta ya afya kutoka shilingi bilioni 300 2005/2006 hadi shilingi trilioni 1.2
mwaka 2011/12 na imekuwa ya tatu baada ya miundombinu na elimu.
Tumeziimarisha hospitali za Mikoa kwa vifaa tiba na wataalamu wa afya.
Kazi inaendelea katika hospitali za Wilaya. Tumewekeza katika Hospitali
ya Muhimbili. Hospitali hiyo ilivyo leo sivyo ilivyokuwa miaka sita
nyuma. Na kazi inaendelea hasa katika maeneo ambayo tunapeleka wagonjwa
nje. Matunda yake yanaanza kuonekana kwa upande wa figo, moyo, kinywa
na mipango inaendelea kwa upande wa ubongo na mishipa ya fahamu.
Tunaendelea kuimarisha mafunzo ya madaktari na madaktari bingwa, yote
kwa nia hiyo hiyo.
Hivi sasa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba,Muhimbili kinachukua wanafunzi
wengi zaidi ya ilivyokuwa siku za nyuma na makazi mapya ya chuo
yanaendelea kuandaliwa ili kuchukua wanafunzi wengi zaid. Mwaka 2005
tulikuwa na madaktari bingwa 46 mwaka huu tunao 520.
Ndugu Wananchi;
Jambo la tano ambalo pande zote mbili zilikubaliana ni kuhusu madaktari waliofukuzwa. Hawa ni wale Interns
waliokuwa wamerudishwa Wizarani kutoka Muhimbili na kupangiwa hospitali
za Temeke, Ilala, Mwananyamala na Lugalo. Hili ni jambo ambalo
lilikuwa limemalizika kitambo na wote walikuwa wamerudi Muhimbili.
Jambo la sita
ni kuhusu mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na madaktari kuhusu
kuboresha huduma ya afya. Mapendekezo hayo yalihusu kutathmini sera na
mpango wa afya ya msingi, bajeti ya afya kuwa asilimia 15
ya bajeti ya Serikali, kuwepo na utaratibu mzuri wa kuajiri madaktari
na kuboresha viwango vya ubora wa madaktari na kadhalika. Serikali
imeyaafiki mapendekezo hayo na yatafanyiwa kazi.
Jambo la saba,
ambalo pande zote walilokubaliana ni kuhusu kuongeza posho ya uchunguzi
wa maiti. Hili ni jambo jipya halikuwepo mwazoni. Hata hivyo,
Serikali imelikubali na posho hiyo imeongezwa kutoka shilingi 10,000/=
hadi kufikia shilingi 100,000/= kwa daktari na shilingi 50,000/= kwa wasaidizi wake.
Ndugu Wananchi;
Kuna masuala matatu ambayo yamekuwa na muafaka kwa kiasi fulani na kutoafikiana kwa baadhi ya mambo. La kwanza
ni suala la kufanya kazi katika mazingira hatarishi. Serikali
imekubali hoja ya kuchukua hatua ya kuwalinda madaktari wanaofanya kazi
katika mazingira hatarishi. Serikali iliwaeleza kuwa watumishi wa kada
zote za afya watapatiwa chanjo dhidi ya maambukizi ya Hepatitis B na fedha zimetengwa katika bajeti ya 2012/13.
Aidha,
Serikali imeeleza dhamira ya kurudisha posho ya mazingira hatarishi kwa
watumishi wa umma wanaostahili. Utekelezaji wake utafanyika baada ya
uchambuzi wa kina wa kubainisha mazingira hatarishi ni yepi, viwango
stahiki viwe vipi na nani hasa wahusike. Madaktari wamekataa hili la
kufanya uchambuzi, wanataka kiwango kiwe kama wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya mshahara na kianze mara moja.
Jambo la
pili ambalo wamekubaliana nusu nusu ni kuhusu nyumba za kuishi.
Serikali imekiri wajibu wake wa kuwapatia madakari nyumba za kuishi.
Aidha, imeeleza mpango ulioanza wa kujenga nyumba 700 za madaktari kote nchini na kwamba hivi sasa ujenzi wa nyumba 90 unaendelea, 50 katika mkoa wa Mtwara na 40 katika mkoa wa Rukwa.
Kwa maeneo ambayo madaktari wanalipwa posho ya pango Serikali imesema
waajiri wataendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizopo kwa
watumishi wa umma wenye stahili ya kupewa nyumba. Jambo hilo
limekataliwa na Madakari na kutaka lazima walipwe asilimia 30
ya mshahara kama posho ya nyumba. Serikali kwa upande wake imeona
vigumu kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa wafanyakazi
wengine wote wa umma.
Jambo lingine
ambalo lilikuwa na makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu posho ya kufanya
kazi katika mazingira magumu. Pande zote mbili ziliafikiana kuwa yapo
baadhi ya maeneo nchini yanayo mazingira magumu kwa watumishi wa umma
hivyo hatua zichukuliwe kuwasaidia watumishi hao. Serikali imekubali
wajibu wa kuweka utaratibu wa kuboresha maisha ya watumishi katika
maeneo hayo. Kwa ajili hiyo, Serikali itatoa mwongozo kwa mamlaka za
ajira kuhusu namna ya kuwasaidia watumishi hao kupunguza makali ya
maisha katika kila eneo badala ya kutegemea posho peke yake.
Kuhusu posho, Serikali imeeleza kuafiki kuwepo posho ya aina hiyo ila
itatekelezwa baada ya kufanya uchambuzi wa kuainisha mazingira husika,
kutambua watumishi waliopo na gharama zake.
Madaktari hawajakubali kusubiri zoezi la uchambuzi lifanyike, wanataka
Serikali ilipe posho hiyo sasa. Tofauti hapa si posho hiyo kuwepo, bali
ni rai ya Serikali ya kubaini maeneo yenyewe na kupanga aina ya hatua
na viwango vya posho kulingana na mazingira halisi ya maeneo. Madaktari
hawaoni haja ya kufanya hayo.
Ndugu Wananchi;
Mambo mawili hayakuwa na muafaka kabisa kati ya pande zetu mbili.
Jambo la kwanza ni posho ya kuitwa kazini (on call allowance). Kwanza
sina budi kueleza kuwa Serikali imekubali kuongeza posho hiyo. Tangu
Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi shilingi 25,000/= kwa daktari bingwa (Specialist), shilingi 20,000/= kwa dakari mwenye usajili wa kudumu (Registrars) na shilingi 15,000/=
kwa madaktari waliohitimu ambao wapo katika kipindi cha mafunzo kazini
(Interns). Viwango hivyo vya posho vinatumika hivi sasa.
Madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza walipwe asilimia 10
ya mshahara. Ugumu wa kukubali pendekezo la madakari ni kuwa sharti la
malipo haya ni mtu kuitwa kazini. Ukitaka ilipwe kiwango cha mshahara
ina maana kuwa hata kama daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa na
hakutokea aendelee kulipwa. Hili haliwezi kuwa sahihi kufanya.
Linaweza kuwafanya baadhi ya madaktari kutokutimiza wajibu wao kwa vile
wana hakika mwisho wa mwezi malipo yako pale pale.
Ndugu Wananchi;
Jambo
la pili ambalo muafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari ni
kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari. Madaktari wanataka uwe shilingi 3,500,000/= wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi. Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia 15 mpaka 20
kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika mwaka huu wa
fedha. Kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari ataanzia kati ya shilingi 1,100,000/= na 1,200,000/= kutegemea kiwango kipi hatimaye kitaamuliwa. Madaktari wamekataa katakata na wameng’ang’ania shilingi 3,500,000/=.
Ndugu Wananchi;
Huo
ndiyo mlolongo wa mambo yaliyozungumzwa na pande zote
mbili na matokeo ya mazungumzo yenyewe. Katika kikao cha sita
kilichofanyika tarehe 30 Mei, 2012, upande wa Chama cha Madaktari
ulisema kuwa kwa vile hoja ya nyongeza ya mshahara haina mabadiliko
hawakuona haja ya kuendelea na majadiliano mpaka watakapowasiliana na
wenzao. Waliahidi kutoa taarifa ndani ya wiki mbili. Tarehe 12 Juni,
2012, Rais wa MAT aliandika barua kwa Katibu Mkuu Utumishi ambaye ndiye
kiongozi wa majadiliano kwa upande wa Serikali, kuwa Madaktari
wameikataa taarifa na ufafanuzi waliopewa kutoka Serikalini kwa ujumla
wake.
Ndugu Wananchi;
Baada ya majibu yale ya madaktari, tarehe 19 Juni, 2012, Serikali na
Madaktari walikwenda kwa Msuluhishi (CMA) kutoa taarifa kuwa mgogoro
umekosa usuluhishi kama sheria inavyotaka. Kwa pamoja pande zote mbili
zilikubaliana suala hilo lifikishwe Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi.
Wakati pande zote zinasuburi mgogoro huu kufikishwa ngazi hiyo ya
juu, upande wa Madaktari ukatangaza kuwepo kwa mgomo kuanzia saa sita
ya usiku tarehe 23 Juni, 2012. Hatua hiyo haikustahili kwani suala
lenyewe halijafika mwisho wa kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria za
Mahusiano ya Kazi nchini.
Ndugu Wananchi;
Tarehe
22 Juni, 2012, Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaenda Mahakama Kuu
Kitengo cha Kazi kulifikisha suala la tishio la mgomo na kuomba zuio la
muda kufanywa. Mahakama Kuu ilikubali ombi hilo na kuagiza kuwa mgomo
usitishwe. Juhudi za kumtafuta Rais wa MAT, Dkt. Namala Mkopi na
viongozi wengine wa MAT hazikufanikiwa, Ofisi ya MAT ilikuwa imefungwa
na simu zote za viongozi wa MAT zilikuwa
zimezimwa. Hatimaye tarehe 25 Juni, 2012, alipatikana na kupewa amri
hiyo ya Mahakama. Tarehe 26 Juni, 2012, Dkt. Mkopi alifika Mahakamani
ambapo alikana kuwa yeye hahusiki na kuitisha huo mgomo lakini hakumtaja
aliyehusika. Pamoja na rai hiyo, Jaji alimuamuru Rais wa MAT
akawatangazie wanachama wake kusitisha mgomo. Dkt. Namala Mkopi
hajafanya hivyo hadi leo na mgomo umekuwa unaendelea kinyume cha Sheria.
Ndugu Wananchi;
Wagonjwa
wanateseka na wengine kupoteza maisha kwa mgomo huu usiokuwa halali
kisheria ambao pia haustahili kuwepo hata kwa mujibu wa maadili ya
udaktari. Viongozi wa MAT na wenzao wanawaingiza Madaktari katika
mgogoro na Mahakama na waajiri wao isivyostahili. Ni vyema viongozi wa
Madaktari na madaktari wakatambua kuwa
wanashiriki katika mgomo usiokuwa halali ambao pia kiongozi wao mkuu
amekana Mahakamani kuwa hahusiki nao. Madaktari lazima watambue pia
kwamba ajira zao wanaziweka hatarini.
Mfanyakazi ana kinga ya kutofukuzwa kazi na mwajiri kwa kushiriki mgomo
unaokubalika kisheria. Huu siyo. Watapoteza ajira, hawana pa
kukimbilia, hawana cha kiwalinda. Kwa madaktari interns, wanahatarisha
maisha yao kwani hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki mgomo usiokuwa
halali. Lazima watafakari sana kwa hayo wafanyayo.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kurudia maneno niliyoyasema tarehe 12 Machi, 2012, kuwa kuboresha
mishahara na maslahi ya wafanyakazi ni Sera ya Serikali yetu kwa
maelekezo ya Ilani ya Chama Tawala (CCM).
Tumeitekeleza kwa vitendo sera hiyo, hata hivyo ni ukweli ulio wazi
kuwa nia yangu njema tu pekee haitoshi, lazima uwezo wa kufanya hivyo
uwepo. Kwa kulingana na uwezo uliopo, tumeendelea kuboresha
mishahara na maslahi ya wafanyakazi hatua kwa hatua tangu tuingie
madarakani. Tumefanya hivyo kwa jumla kwa wafanyakazi wote na kwa kada
mbalimbali za watumishi wa umma.
Miongoni
mwa wafanyakazi wa umma walionufaika na hatua
hizo za Serikali ni madaktari na watumishi wa kada nyingine za huduma
ya afya. Tena nadiriki kusema madaktari tumewapa upendeleo mkubwa
kuliko watumishi wengine wa umma. Upendeleo upo kwenye mafunzo ambapo
wanafunzi wa udaktari wanagharimiwa na Serikali kwa asilimia mia moja
wakati wanafunzi wenzao wa taaluma nyingine hawako hivyo.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2004/2005, mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa shilingi 178,700/=, mwaka 2005/ 2006 tuliupandisha na kuwa shilingi 403,120/=. Tuliendelea kuupandisha mwaka hadi mwaka mpaka kufikia shilingi 957,700/=
wanazolipwa sasa. Kiasi hicho ni mara mbili ya mishahara ya watumishi
wa taaluma nyingine wenye shahada ya kwanza wanaoanza kazi ambao kwa
wastani hupata shilingi 446,100/=.
Tunafanya
hivyo kwa kutambua na kuthamini nafasi maalum ya madaktari katika jamii
na ukweli kwamba bado tunayo safari ndefu ya kuziba pengo la madaktari
nchini. Lakini inaonekana juhudi zetu zote hizo hazithaminiwi.
Ndugu Wananchi;
Sina
budi kusisitiza kwamba tunapofanya hivyo tunaongozwa na uwezo tulio
nao wa kulipa. Kwa sasa hatuwezi kuwaahidi kuwa tunao uwezo wa
kuwalipa mshahara wa kuanzia wa shilingi 3,500,000/= na posho zote zile. Tukifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa shilingi 7,700,000/=. Kwa hakika kiasi hicho hatutakiweza. Si vyema kutoa ahadi hewa kwa watu tunaowaheshimu na kuwathamini kama walivyo madaktari.
Kutokana
na ukweli huo basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi
Serikalini bila ya kulipwa mshahara huo awe huru kuacha kazi na kwenda
kwa muajiri anayeweza kumlipa kiasi hicho. Nasi tutamtakia kila la
heri. Hana sababu ya kugoma ili ashinikize kulipwa mshahara huo.
Asisumbuke,
hatalipwa mshahara huo. Isitoshe, hana sababu ya kuendelea kuwa na
mgogoro na mwajiri ambaye hana uwezo wa kumlipa anachokitaka. Huna
sababu ya kumpa usumbufu mwajiri wa kukuandikia barua ya kujieleza au
kukuachisha kazi. Kwa nini upate usumbufu wa kupata barua hizo na
kuzijibu. Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa
kuondoka kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24. Jiepushe na yote
hayo kwa kujiondoa mwenyewe. Usipofanya hivyo, mwajiri anakuwa hana
jinsi bali kukuondoa kazini maana unakwenda kinyume na sheria za kazi na
maadili ya kazi ya udaktari.
Mamlaka za ajira zimeanza kuchukua hatua hizo na wataendelea kufanya
hivyo kwa wote wanaoendelea kugoma. Najua
baada ya hatua hizo kuchukuliwa kuna manun’guniko ya kuonewa. Hivyo,
mlitegemea mwajiri afanyeje? Ni bora kufanya hivyo ili ajue hana daktari
aweze kufanya utaratibu wa kuziba hilo pengo na huyo ajae awe na mahali
pa kuishi. Vinginevyo atakuwa anajidanganya kuwa anae daktari ambae
hayupo kazini na wala hataki kufanya kazi.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuwathibitishia kwamba dhamira ya Serikali ya kuboresha maslahi ya
watumishi wa umma wakiwemo
madaktari iko wazi. Tumekuwa tunafanya hivyo, na tutaendelea kufanya
hivyo kulingana na uwezo wa kibajeti. Ni vyema watumishi wa umma
wakatambua kuwa hatuwezi kutumia fedha zote au kiasi kikubwa mno cha
pesa za umma kulipana mishahara. Tukifanya hivyo, Serikali itashindwa
kutoa huduma muhimu kwa wananchi ambao ndiyo wengi na wanastahili
kuhudumiwa. Hata hizo huduma za afya tunazosema ni duni tuziboreshe,
hatutaweza kuziboresha kama tutatumia sehemu kubwa ya pesa za Serikali
kuwalipa mishahara wafanyakazi.
Hivi sasa matumizi ya mishahara ni asilimia 48 ya bajeti ya Serikali. Kiwango hicho ni kikubwa mno. Uwiano mzuri ni kuwa na matumizi ya mishahara yasiyozidi asilimia 35 ya bajeti na asilimia 65 zitumike kugharimia huduma na shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi na taifa. Sisi tumezidi kwa asilimia 13. Hivyo, hatuna budi tukubali kujinyima kwa manufaa ya walio wengi.
Suala la Dkt. Steven Ulimboka
Ndugu Wananchi;
Kabla
ya kumaliza hotuba yangu, napenda kuungana na Watanzania wenzangu wote
kuelezea masikitiko yangu makubwa na kuhuzunishwa kwangu na kitendo cha
kinyama alichofanyiwa Dkt. Steven Ulimboka usiku wa tarehe 26 Juni,
2012. Kitendo hicho ni kinyume kabisa na mila na desturi zetu.
Watanzania hatujayazoea mambo hayo.
Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa
kina ili ukweli ujulikane. Nimesema kuwa ningependa ukweli huo
ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana shaka na kulaumiana
kunakoendelea hivi sasa.
Natambua
kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka. Mimi
nimeshangazwa sana na
hisia hizo kwani siioni sababu ya Serikali kufanya hivyo. Dkt.
Ulimboka alikuwa mmoja wa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya
Serikali na Madkatari. Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali,
hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya. Kulikuwa na rai ya
kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam Madaktari wanamuamini
kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na
Serikali.
Ndugu Wananchi;
Kama
nilivyoeleza, mazungumzo yalienda vizuri na mafanikio makubwa
yamepatikana. Yapo maeneo machache na hasa eneo la mshahara ambalo
hatukuweza kukubaliana. Hapo tulipofikia si pabaya na tulikubaliana
sote kurudi kwenye mkondo wa Sheria kusaidiwa. Kwa nini Serikali
imdhuru Dkt. Ulimboka? Na, kuhusu mgomo, Mahakama Kuu imekwishatoa amri
ya kusitisha mgomo. Anayekaidi amri ya Mahakama ananunua ugomvi na
mhimili huo wa dola ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu mtu huyo.
Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dkt. Steven
Ulimboka kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru? Kama kuna
mtu wa Serikali kafanya, itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za
Serikali au kwa kutumwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;
Kwa
niaba yangu na kwa niaba ya Serikali natoa mkono wa pole kwa Dkt.
Steven Ulimboka na kumuombea apone haraka ili aungane na familia yake na
Watanzania wenzake katika ujenzi wa taifa. Kwa namna ya pekee
namshukuru na kumpongeza Bwana Juma Mgaza, kwa moyo wake wa huruma na
upendo na kwa hatua alizochukua za kumsaidia Dkt. Ulimboka.
Naomba
kumaliza kwa kuwasihi madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini.
Watanzania wenzenu wanateseka na kupoteza maisha. Muwe na moyo wa
huruma na upendo na msaada kwa wagonjwa kama kiapo chenu kinavyowataka.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.